Tuesday, 14 June 2016

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA AIPONGEZA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA KWA MIKAKATI YA KUTATUA UPUNGUFU WA MADAWATI


Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima akizindua mpango wa ugawaji wa madawati katika shule za Wilaya ya Mbinga; mpango huu ni utekelezaji wa agizo la mheshimiwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa John Pombe Magufuli
WILAYA ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetenga zaidi ya shilingi milioni 475.8 kwa ajili ya  kukabiliana na upungufu wa madawati, meza na viti  kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli, alilotoa hivi karibuni wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa  na kuzitaka halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha zinamaliza tatizo hilo.
Aidha wilaya hiyo tayari imefanikiwa kutengeneza madawati 6,134 kati ya madawati 12,952 ambapo kwa shule za msingi madawati yaliyokamilika ni 3,634 na shule za sekondari 2,500 sawa na asilimia 47.6 ya lengo kwa gharama ya shilingi milioni 169 na tayari yamekwisha sambazwa kwenye shule husika, huku mchakato wa kumaliza madawati 5,510 kwa shule za msingi 3,810 na sekondari 1,700 ukiwa katika hatua ya mwisho kukamilika kwake.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga vijijini, Venance Mwamengo wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa, George Mbijima katika kijiji cha Mbuji kata ya Mbuji wilayani humo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa,  George Mbijima akiangalia ubora wa meza na madawati juzi katika kijiji cha Mbuji wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kabla ya kusambazwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani humo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mtendaji alieleza kuwa kiasi hicho cha fedha ni gharama za kununulia mashine za kuranda, kukata na kukunja vyuma, mashine za kupasulia mbao, umeme na gharama zingine ndogo ndogo na kwamba madawati hayo yametengenezwa kwa kutumia mbao pamoja na chuma ili yaweze kuwa imara tofauti na madawati yanayotengenezwa kwa mbao tupu, ambayo huharibika kwa haraka na hayadumu kwa muda mrefu.

Mkurugenzi mtendaji alisema kuwa wilaya hiyo yenye halmashauri mbili ya Mbinga mjini na Mbinga vijijini  ilikuwa na upungufu wa madawati 12,952 ambayo katika shule za msingi upungufu ulikuwa madawati 8,452 viti na meza kwa shule za sekondari upungufu ulikuwa 4,500 ambapo katika utekelezaji wa agizo la serikali walianza kutengeneza madawati mwezi Januari mwaka huu na kwamba wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Alisema kuwa mradi wa kutengeneza madawati ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, ulianzishwa ili kutekeleza agizo la serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika kuhakikisha kwamba halmashauri zinapunguza kero hiyo ya upungufu wa madawati, ili kuweka mazingira mazuri ya kusomea wanafunzi na walimu kufundisha watoto wanapokuwa darasani.
Kwa upande  wake kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa George Mbijima, amewapongeza viongozi wa wilaya hiyo kutokana na jitihada wanazozifanya pamoja na ubunifu wa miradi mingi na mizuri ya maendeleo ya wananchi, ambayo  imejengwa  kulingana na thamani halisi ya fedha.
Mbijima amewataka  wananchi, watumishi na viongozi wa serikali wilayani Mbinga, kutobweteka na mafanikio waliyonayo badala yake waongeze juhudi katika kufanya kazi na viongozi kutumia muda mwingi kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.
Katika hatua nyingine aliwaagiza wahakikishe pia wanashirikisha makundi ya vijana katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Wapeni kipaumbele vijana ili nao waweze kutambua wajibu wao, mkifanya hivi ni hatua nzuri itakayosaidia kuongeza juhudi katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili, kama vile ukosefu  mitaji kwa ajili ya  kuanzisha miradi ya kiuchumi”, alisema Mbijima.
Vilevile kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kitaifa, amewataka wazazi na walezi wilayani humo kushirikiana na serikali katika kutatua tatizo la upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari, ili kuwawekea mazingira mazuri watoto wao wanapokuwa darasani waweze kupenda kusoma na kufanya vizuri katika mitihani yao.
Pia ameviagiza vyombo vya dola kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani wanaume wenye tabia ya kuwarubuni wasichana ambao bado wanasoma shuleni kwa kufanya nao mapenzi, kwa sababu wamekuwa chanzo kwa wasichana wengi hapa nchini kukatisha  masomo yao.